Mtu Aliye Makini kuhusu Matendo Yake

Baadhi ya watu hubadilisha msimamo kwa urahisi kulingana na maneno ya marafiki au majirani zao. Hufuatilia sana uvumi kuhusu wengine, hueneza uvumi huo kwa watu wengi na kusababisha wahusika wahukumiwe na kulaumiwa. Rafiki yao wa karibu akisema uwongo, wanaamini na hatimaye hujikuta katika matatizo.

Hili linaonyeshwa katika 2 Wafalme 12 kupitia habari za Yoashi, mfalme wa Yuda. Wakati warithi wote wa kifalme walipouawa, Yoashi aliokolewa kwa shida, kisha akapandishwa kwenye kiti cha enzi kwa msaada wa kuhani Yehoyada. Mwanzoni Yoashi alifanya yaliyo mema machoni pa Mungu siku zote za kuhani Yehoyada. Lakini baada ya Yehoyada kufa, mfalme aliwasikiliza maafisa waovu wa Yuda waliokuja na kumsujudia.

Mfalme na maafisa wake walimwacha Mungu na kuabudu sanamu. Ghadhabu ya Mungu ikawajia watu wa Yuda, nao wakavamiwa na jeshi la Waaramu. Ingawa jeshi hilo lilikuwa na watu wachache, Mungu alitia mikononi mwao jeshi kubwa sana la Yuda. Mfalme Yoashi akauawa na watumishi wake mwenyewe waliokula njama dhidi yake. Mtu mpumbavu huelekezwa huku na huku kwa urahisi na maneno ya wengine, na hushindwa kuzaa matokeo mema.

Mtu mwenye moyo mwema hatikiswi na maneno ya watu waovu, wala hawahukumu wengine kabla ya kujionea mwenyewe na kupata uzoefu wa moja kwa moja. Hata anapojionea, hasambazi mambo anayojua kwa wengine. Mithali 14:15 inasema, “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” Hata maneno yaleyale yakisemwa, tafsiri yake hutofautiana kulingana na msemaji. Maana ya neno moja pia inaweza kubadilika kulingana na kiimbo, msisitizo na kasi ya kusema.

Kwa hiyo, ni upumbavu mkubwa kuwahukumu au kuwalaumu wengine kwa kutegemea tu maneno uliyoambiwa na mtu mwingine. Ukichukua hatua bila kufikiri na kwa uzembe kutokana na uliyosikia, unaweza kukumbana na makosa au misiba isiyoweza kurekebishwa. Ninaomba kila mmoja ajiepushe na upumbavu wa kuwashuku, kuwahukumu na kuwalaumu wengine kwa kusikia tu maneno ya watu; badala yake atende kwa hekima na busara katika kila jambo. Ninaomba haya katika jina la Bwana wetu!

    His Emeritus Bishop Dr. Jaerock Lee

Word of Life